Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa,
Mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya si ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa au Jeshi la Polisi peke yake bali ni jukumu la jamii nzima. Kwa kutambua hilo TAKUKURU na Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Elimu kwa Umma imeamua kushirikisha jamii nzima katika mapambano haya ikiwa ni pamoja na wanafunzi waliopo shuleni kwa kuunda klabu za wapinga rushwa na dawa za kulevya. Shughuli za Klabu hii ni pamoja na kuhamasisha jamii nzima katika mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya kwa njia ya Nyimbo, Ngonjera, Maigizo, Uandishi wa Insha na Uchoraji wa Katuni.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa,
Lengo la kuunda Klabu ya wapinga Rushwa na dawa za kulevya katika shule ya sekondari Mpui ni kuwafanya wanafunzi hao waelewe ubaya wa rushwa ili waichukie na kupambana nayo, na vilevile wajue madhara ya dawa za kulevya tangu wakiwa wadogo ili waepukane nayo na hatimaye kuwa na kizazi chenye nguvu kwa maendeleo ya Taifa. Pia, kujenga uelewa kuhusu mapambano dhidi ya Ukimwi na umuhimu wa Lishe bora kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa,
Matarajio yetu katika kufungua klabu hii ni kuleta chachu ya kujenga kizazi kisichoweza kuvumilia wala kukumbatia rushwa na dawa za kulevya katika kutekeleza majukumu yake. Pia kupata watumishi na viongozi waadilifu wa sekta mbalimbali, hatimaye kupunguza vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya dawa za kulevya katika jamii.
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa,
Wahusika wa mradi ni wanafunzi wanachama wapatao 40 kati yao wavulana ni 15 na wasichana ni 25 wakiongozwa na mwalimu mlezi kwa kushirikiana na viongozi wanafunzi.
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa tunaomba utufungulie klabu hii.
MRADI WA MAJI KALAMBAZITE
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Tunayo furaha kukukaribisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kata ya Kalambazite, Kijiji cha Kalambazite katika mradi huu wa Maji.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Ujenzi wa Mradi wa Maji Kalambazite unatekelezwa na wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza unatekelezwa katika vijiji vya Kalambazite, Mleche, Mshani na Kilembo vya Kata ya Kalambazite, na itahusisha ujenzi wa kisima cha pampu (sump well), ufungaji wa pampu, uunganishaji wa umeme umbali wa kilometa 3, uunganishaji wa mtandao wa mabomba kilometa 30.7, ujenzi wa matanki matatu yenye mita za ujazo 1000, 300 na 225 na ujenzi wa vituo 39 vya kuchotea maji. Aidha awamu ya pili itahusisha kupeleka maji katika vijiji vitatu vya Ikozi, Chituo na Tentula katika kata ya Ikozi umbali wa kilometa 6.8 na awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Mkandarasi anayetekeleza awamu ya kwanza ya mradi huu anaitwa KOBERG CONSTRUCTION LTD JV ANDIC LTD kwa mkataba namba AE-102/2021-2022/RKW/W/31 kwa gharama ya shilingi 6,078,570,326.61/= kwa muda wa siku 270 na ulitakiwa kukamilika tarehe 22 Februari 2023. Hata hivyo Mkandarasi ameongezewa muda wa siku 240 kutokana na changamoto za mvua na mabadiliko ya usanifu wa mradi na sasa mradi utakamilika tarehe 24 Oktoba 2023. Hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60.7 na Mkandarasi ameshalipwa shilingi 1,915,809,244.09.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Hadi awamu ya kwanza ya mradi utakapokamilika, wananchi 16,030 watanufaika na huduma ya maji safi na salama katika kata ya Kalambazite na itakapokamilika awamu ya pili na ya tatu ya ujenzi wa mradi, jumla ya wananchi 27,958 wa kata hiyo watanufaika. Manufaa mengine ya mradi ni kuwa wananchi hawatapata adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na upatikanaji huo wa maji utaboresha na kuimarisha Afya za Wananchi kwa sababu maambukizi ya magonjwa ya milipuko yatapungua. Kwa mantiki hiyo na gharama za matibabu zitapungua.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Kwa heshima na taadhima, sasa tunaomba ukague miundombinu ya Mradi wa Maji na utuwekee jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji Kalambazite.
UTOAJI WA MOTISHA KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI ZILIZOFANYA
Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ina jumla ya shule za Msingi 113 ikiwa shule za serikali 112 na binafsi 1, na kituo 1 cha kutolea mafunzo kazini kwa walimu. Pia Halmashauri ina shule za Sekondari 25 kati ya hizo shule 19 ni za Serikali na 6 ni za binafsi. Shule 19 ni za kidato cha kwanza hadi cha nne na shule 5 ni za kidato cha kwanza hadi cha sita, kati yake 4 ni za serikali na 1 ni ya binafsi.
Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa
Hali ya taaluma katika Halmashauri hii imeendelea kuwa ya kuridhisha kutokana na kuboreshwa ufaulu wa mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi, kwa mfano kwa mwaka 2020 ufaulu ulikuwa 73.22% na mwaka 2021 ufaulu ulikuwa 73.52. Kwa upande wa Shule za Sekondari kidato cha IV kwa mwaka 2020 ufaulu ulikuwa 88.7% na mwaka 2021 ufaulu ulikuwa 94%. Vigezo vilivyotumika kupata shule zilizofanya vizuri ni ufaulu wa asilimia 97 hadi 100 kwa upande wa sekondari na shule zilizofanya vizuri kwa wastani wa 189 hadi wastani wa 224.49 upande wa shule za msingi.
Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa
Manufaa ya utoaji wa Motisha ni kama ifuatavyo:-
Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa
Tunaomba ukabidhi zawadi zenye thamani ya shilingi 2,000,000.00 na kuwapatia Vyeti vya pongezi Walimu wa shule za Msingi Ilemba, Tuwi, Kipeta, Rukwa, Mukamanye na kwa Wakuu wa shule za Sekondari Kipeta, Kikwale, Kapenta, Kaoze, Makuzani, Unyiha, Mpui, Vuma na Uchile.
UJENZI WA JENGO LA WAGONJWA WA NJE (OPD) KITUO CHA AFYA KAENGESA (MAPATO YA NDANI)
Ndugu kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Ujenzi huu wa kituo cha Afya Kata ya Kaengesa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 ibara ya 83 (d) ambayo inaelekeza kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za Afya ili viweze kutoa huduma Bora zaidi kwa wananchi.
Ndugu kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Kata ya Kaengesa ni miongoni mwa Kata 27 za Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, na ina jumla ya vijiji 4, vitongoji 16 vyote kwa ujumla vikiwa na Idadi ya kaya 3,289, zenye jumla ya watu 14,952 ikiwa wanawake ni 7,106 na wanaume 7,846. (Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022).
Eneo ambalo mradi huu unajengwa lina ukubwa wa Ekari 6.1 ambazo zinakidhi miundombinu ya Kituo cha Afya, limepimwa na liko kwenye plot namba 83 Block B-Kaengesa.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Mradi huu wa Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kaengesa unatekelezwa kwa Fedha kutoka Mapato ya ndani (OWN SOURCE) shilingi milioni mia mbili sabini na tano (TZS: 275,000,000.00) ambazo ndio za mkataba halisi, aidha wananchi wamechangia ardhi yenye thamani ya 4,880,000 na kufanya jumla ya gharama zote za mradi kuwa shilingi 279,880,000 hadi kukamilika kwa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Utekelezaji wa mradi unafanywa na mkandarasi HYUDAVIS Company LTD.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Ujenzi wa Kituo hiki cha Afya cha kimkakati utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia wananchi 39,554 waishio katika Kata tatu za Kaengesa, Lyangalile na Kanda na wale wanaoishi maeneo ya jirani. Huduma za akina mama wajawazito na watoto zitaimarika na kupunguza kero kwa wananchi.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Kwa heshima na taadhima tunaomba sasa ukague na utuwekee jiwe la msingi katika mradi wetu.
UPANDAJI MITI KATIKA SHULE YA MSINGI TUWI B
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga inatekeleza agizo la upandaji miti Kitaifa ambalo linaelekeza kupanda miti milioni moja na laki tano (1,500,000) kila mwaka.
Upandaji miti unafanywa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo jamii, Taasisi za Serikali zikiwemo shule za Msingi na Sekondari, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia mradi wa kurejesha Mazingira yaliyoharibika, TASAF na taasi sizisizo za Kiserikali zikiwemo Timu ya Wanasheria watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Shirika la Maendeleo endelevu Rukwa (RUSUDEO) na Shirika la Hifadhi ya Mazingira la Kaengesa(KAESO). Zoezi la upandaji miti linafanyika katika kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kutunza Mazingira na Kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Katika Msimu wa Mwaka 2022/2023 Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanda jumla ya miti 1,022,000 ambayo ni sawa na asilimia 68 ya lengo la upandaji wa miti 1,500,000. Pamoja na miti iliyopandwa, tuna vitalu 3 vyenye jumla ya miche 120,000 katika vijiji vya Ilemba, Solola na Sakalilo ambayo tunatarajia kupanda miti hiyo mwezi Novemba wakati wa mvua za masika zitakaporejea.
Katika kuendelea kutekeleza agizo la upandaji wa miti Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwa kipindi cha kuanzia tarehe 2/4/2023 – 1/9/2023 miti iliyopandwa ni 1,300 na miti inayopandwa wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Halmashauri yetu ni miti 520.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Miti 320 imepandwa katika Kituo cha Afya Kaengesa, Miti 1,000 Shule ya Msingi Tuwi A na B, na miti 500 shule ya msingi Tuwi B ambayo inapandwa siku ya Mwenge ukiwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Gharama za mradi wa upandaji miti katika mbio za Mwenge mwaka 2023 ni Tshs. 2,490,000 ambazo zinajumuisha miti iliyopandwa kituo cha Afya Kaengesa, shule za msingi Tuwi A na B
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Tunaomba muungane nasi kwa kupanda miti 500 katika shule ya msingi TUWI B ikiwa ni jitihada za kuendelea kuhamasisha jamii kupanda miti na kutunza Mazingira.
KAMYALILE SOAP MAKING GROUP
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Halmashauri imekuwa ikitenga asilimia kumi ya Mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 ibara ya 32(S). Katika kipindi cha Mwaka 2022/2023 kikundi kilikopeshwa Tsh. 20,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kutengenezea sabuni na malighafi zake. Kikundi kina idadi ya wanakikundi 5 wanaume wakiwa 3 na wanawake 2.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Mradi huu umegharimu shilingi 24,445,000 ambapo shilingi 20,000,000 ni Mkopo toka Halmashauri na shilingi 4,445,000 ni fedha inayotokana na michango ya wanakikundi. Fedha hizi zimetumika kununua mashine za kutengeneza sabuni, malighafi, kuingiza umeme na kugharamia jengo la kiwanda.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Mkopo huu ni wa miezi 36 ambapo hadi kufika leo tarehe 01/09/2023 Jumla ya shilingi 1,112,000 zimerejeshwa, Dhamira yetu ni kumaliza kulipa mkopo wote ndani ya miezi 24. Kuanzia mwezi Mei, 2023 Kikundi kimezalisha sabuni miche 9,800 za shilingi 24,500,000/= ambazo zimewezesha kuendeleza kazi za kiwanda na kulipa posho za wanaKikundi wanaofanya kazi.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Manufaa ya mradi huu ni Pamoja na kuongezeka kwa kipato kwa Mwanakikundi kutoka wastani wa shilingi 50,000 hadi 200,000. Ongezeko hili limetokana na malipo wanayolipwa wanakikundi wanapofanya kazi kiwandani. Pia kiwanda kimetoa ajira kwa watu 32 ambapo 5 wanafanya kazi kiwandani, na walioko kwenye mnyororo wa thamani ni 27. Ongezeko la kipato linasaidia ustawi wa familia zao.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Kwa heshima na taadhima, tunaomba sasa ukague shughuli za kikundi cha ‘Kamyalile Soap Making Group’ ambacho kinaendesha Kiwanda cha Kutengeneza Sabuni.
UJENZI WA SHULE MPYA YA MSINGI TUWI B
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Tunayofuraha kukukaribisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kata ya Ilemba Kijiji cha Ilemba B.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Kijiji cha Ilemba B ni miongoni mwa vijiji 114 vya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kilichopo Kata ya Ilemba, chenye wakazi 8700 ikiwa wanaume ni 3,794 na wanawake ni 4,906 ambapo jumla ya Kaya ni 1938 na vitongoji 5.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Mradi huu ulipata fedha za Boost kutoka serikali kuu kiasi cha shilingi 538,500,000 mnamo tarehe 24/4/2023 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya msingi yenye vyumba vya madarasa 16, matundu18 ya vyoo, kichomea taka kimoja (1) na jengo moja (1) la Utawala. Mradi huu unatekelezwa kwa njia ya force akaunti na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 S eptemba, 2023.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Kipekee sana, tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano waTanzania kwa kuendelea kutuletea fedha za uboreshaji wa miundombinu ya Elimu. Kwa kuona umuhimu huo wananchi wamechangia shilingi 2,000,000 kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Kukamilika kwa ujenzi wa shule mpya ya Tuwi B utapunguza msongamano wa wanafunzi katika shule mama ya TUWI ‘A’ yenye wanafunzi 2436.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa
Kwa heshima na taadhima sasa tunakuomba ukague na utuwekee jiwe la Msingi katika majengo ya shule ya TUWI ‘B’.
KLABU YA KUDHIBITI MALARIA KATIKA SHULE YA SEKONDARI ILEMBA.
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa,
Mapambano dhidi ya malaria si ya Waganga na Wauguzi peke yake bali ni jukumu la jamii nzima. Kwa kutambua hilo Shule ya Sekondari Ilemba imeamua kushirikisha jamii nzima katika mapambano haya ikiwa ni pamoja na wanafunzi waliopo shuleni kwa kuunda klabu ya kudhibiti malaria. Shughuli za klabu hii ni pamoja na kuhamasisha jamii nzima katika mapambano dhidi ya mazalia ya mbu wanao sababisha ugonjwa wa malaria, kuhamasisha matumizi ya vyandarua vyenye dawa na kuhamasisha kwa njia ya Nyimbo, Ngonjera, Maigizo, Uandishi wa Insha na Uchoraji wa Katuni.
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa,
Wahusika wa mradi ni wanafunzi wanachama wapatao 57 kati yao wavulana ni 25 na wasichana ni 32 wakiongozwa na mwalimu mlezi kwa kushirikiana na viongozi wanafunzi.
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa,
Lengo la kuunda klabu ya Kudhibiti Malaria katika shule ya sekondari Ilemba ni kuwafanya wanafunzi hao waelewe madhara ya ugonjwa wa malaria ili wachukue hatua za kupambana na ugonjwa huo.
Ndugu Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa,
Matarajio yetu katika kufungua klabu hii ni kuleta chachu ya kujenga kizazi chenye afya bora na kisicho kuwa na malaria, hasa ukizingatia ukanda huu wa Bonde la Ziwa Rukwa kuna mlipuko wa Malaria mara kwa mara. Pia lengo la kuundwa kwa Klabu hii ni ili kupata nguvu kazi isiyokuwa na maambukizi ya Malaria.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa,
Ikiwa ni mwendelezo wa mapambano dhidi ya Malaria katika Halmashauri yetu, tunaomba utufungulie Klabu yetu ya Malaria na kugawa vyandarua ikiwa ni moja ya kinga ya Malaria katika familia na Taifa kwa ujumla.
JENZI WA DARAJA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA MAWE (STONE ARCH BRIDGE)
Utangulizi
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Wilaya Sumbawanga inatekeleza ujenzi wa Daraja kwa kutumia Teknolojia ya mawe ( Stone arch Bridge) yenye midomo mitano (5), urefu wa mita 19.5, upana wa mita 7 na kimo cha mita 1.5. Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi mzawa M/S Migo Builders & Civil Co. Ltd wa S.L.P 192, Sumbawanga.
Jina la Mradi.
Matengenezo ya barabara ya Kalambanzite - Kapoka - Lowe km 5, Ndelema – Kamnyazya km 7.78 na barabara ya Mshani - Mlombo - Ninde km 4.9. Mkataba Na.AE/092/2022-2023/RKW/W/16
Chanzo cha fedha.
Mradi unatekelezwa kwa kutumia fedha za Matengenezo kutoka Mfuko wa barabara (Road Fund)
Utekekelezaji wa Mradi.
Mradi ulianza kutekelezwa kuanzia tarehe 27 Oktoba, 2022 na utakamilika tarehe 30 Septemba, 2023.
Gharama ya Mradi
Gharama ya Mradi wote ni Tzs 200,638,780.00. Kutokana na gharama hizo daraja hili lina jengwa kwa kiasi cha Tzs 48,426,090.00
Kazi zinazotekelezwa.
Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na kuchimba msingi, kumwaga zege, ujenzi wa kuta za mawe na ujazaji wa kifusi ili kuruhusu daraja kupitika.
Manufaa ya Mradi:
Ndugu kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa tunaomba ukague ujenzi wa daraja linalojengwa katika mto Kapoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
SUMBAWANGA
Anwani ya Posta: P.O.BOX 229
Simu ya Mezani: 025-2802133
Simu ya Kinganjani: 0754634811
Barua pepe: ded@sumbawangadc.go.tz
Hati Miliki©2017. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Haki zote zimehifadhiwa