Awali ya yote tunatoa shukrani zetu za dhati kwa kukubali kujumuika nasi katika siku hii muhimu tunapoadhimisha siku ya UKIMWI duniani inayofanyika katika Kata ya Laela tukijumuika na watanzania wenzetu katika Halmashauri mbalimbali nchini kwetu. Kuadhimisha siku hii muhimu ambapo tunawaenzi ndugu zetu waliofariki kwa ugonjwa wa UKIMWI na kuwakumbuka waathirika wa ugonjwa huu, pia kukumbushana kama jamii kuwa ugonjwa huu upo hivyo tuchukue tahadhari.
Maadhimisho haya ya siku ya UKIMWI duniani mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo! “Jamii iongoze kutokomeza ukimwi”
Kupitia kauli mbiu hiyo msisitizo umewekwa ili kutukumbusha kuwa jukumu la mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI ni la dunia nzima, taifa zima na jamii yote zikiwemo asasi mbalimbali, Halmashauri pamoja na mtu mmoja mmoja , hivyo basi tukiungana na kuwajibika kwa pamoja tunaweza kuondokana kabisa na tatizo la UKIMWI katika jamii yetu na kubaki salama bila maambukizi .
Katika kukabiliana na VVU na UKIMWI, Halmashauri imekuwa ikitekeleza malengo ya tisini tano Tatu; (95 AWAMU YA KWANZA): ambapo ifikapo mwaka 2030 asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamepimwa na kujua hali zao za maambukizi ya VVU, (95 YA PILI): Wateja waliogundulika wanaishi na VVU wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU, (95 YA TATU) kati hao wawe wanatumia dawa za kufubuza makali na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI.
Halmashauri tumefanikwa kupunguza maambukizi ya VVU/UKIMWI kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017/2018 hadi kufikia asilimia 4.1 mwaka 2022/2023.
Hali ilivyo kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Viashiria vya VVU na UKIMWI 2022/2023 ni kwamba kwa kiwango cha maambukizi kimepungua toka asilimia 4.4 hadi asilimia 4.1 (KWA MAANA: Kwa asilimia 4.4, kila ukipima watu mia moja lazima ukute watu 4 hadi 5 wana maambukizi ya VVU. Kwa asilimia 4.1 kila ukipima watu mia moja lazima ukute watu 4 wana - maambukizi ya VVU).
Kata zinazoongoza kwa maambukizi ya VVU/UKIMWI ni kata zote za Mwambao wa Ziwa Rukwa na Kata ya Laela.
Sababu kubwa ya kuwa na Maambukizi Makubwa kwenye maeneo hayo ni pamoja na kuwepo kwa wafanyabiashara wengi wa mazao na mifugo hasa nyakati za mavuno ambapo akina Dada wengi wa kujiuza huwepo maeneo haya wakidai wananunua mazao katika maeneo hayo tajwa.
Kwa kata ya Laela hali ya Maambukizi iko juu kutokana na wageni wengi wanaofika maeneo hayo na hasa baada ya kuimarika kwa barabara ya Mbeya, Sumbawanga ambapo magari mengi ya kusafirisha Abiria yanalala Laela na wageni mbalimbali kwa shughuli mbalimbali hapa Laela.
Wapo pia wahamiaji Wafugaji na Wavuvi katika maeneo mbalimbali Mwambao mwa Ziwa Rukwa, wengi wao wakiwa wanatoka Makwao na wakiwa na Maambukizi ya VVU, na wanapofika huku kwetu wanajificha kuweka wazi hali zao za Maambukizi ya VVU kwa Halmashauri yetu ya Sumbawanga.
Tunaamini kupitia hotuba na maelekezo utakayoyatoa leo, yatasaidia kuihamasisha jamii yetu kuweza kuwa na mabadiliko chanya katika kufikia malengo kama halmashauri na jamii nzima tukiwa salama na kusukuma gurudumu letu la maendeleo bila maambukizi.
Tunaipongeza Serikali na wadau wengine wa maendeleo kwa kuwezesha uwepo wa vitendanishi na dawa za kutosha. Katika halmashauri yetu hadi sasa kila kata inatoa huduma ya upimaji, matibabu na malezi ya watu waishio na maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Katika Halmashauri yetu tuna afua mbalimbali za UKIMWI, ambazo zimegawanyika katika makundi makuu matatu ya huduma, ambazo ni:-
Huduma za kuzuia maambukizi (Preventions):
Huduma za upimaji na ushauri nasaa (HTS), Huduma za tohara (VMMC) kwa wanaume na watoto wachanga wa kiume (EIMC), Huduma za uzazi wa mpango, Huduma za ugawaji wa Kondomu, Huduma za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), Huduma za saratani ya shingo ya uzazi (Cervical cancer screening)
Huduma za tiba na ushirikiano (Care and Support):
Magonjwa ya zinaa na via vya uzazi (STIs/RTIs), Huduma za Kifua kikuu na UKIMWI (TB/HIV), Huduma za majumbani kwa wagonjwa waishio na VVU (HBC)
Huduma za tiba na malezi:
Huduma za tiba na malezi (CTC)
Ifuatayo ni taarifa ya huduma za upimaji kwa kipindi cha Oktoba 2022, hadi Septemba 2023; jumla ya wateja 43,347 walipata huduma ya upimaji wa VVU na kati ya hao wanaume 17,980 na wanawake 25,367. Kati yao 973 sawa na 2.2% walikuwa na maambukizi ya VVU ambapo wanaume ni 374 na wanawake 599.
Changamoto
Changamoto zilizoonekana katika utekelezaji wa Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI katika Halmashauri yetu ni kama ifuatavyo:-
Baadhi ya wagonjwa kutohudhuria kliniki kuchukua dawa za kupunguza makali ya VVU yaani ARV kwa sababu ya uoga wa kutengwa na jamii zao, Ukosefu wa elimu kwa baadhi ya wananchi kuhusu ugonjwa huu, Baadhi ya wagonjwa kuto kuwa na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya VVU mfano kuzingatia ulaji wa chakula chenye lishe bora, kutozingatia muda maalumu wa unywaji wa dawa, Mwitikio mdogo wa wananchi kupima afya zao ili kujua hali zao hasa wanaume pindi wenzi wao wakipima basi nawao wanaridhika hali hiyo.
Uhaba wa fedha kwa ajili ya kufanya shughuli za mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
Mapendekezo
Kuendelea kuhamasisha jamii hasa wanaume wajitokeze kwa wingi kupima VVU na sio kwa kuendelea kuridhika na matokeo ya upimaji wa wenzi wao,
Kuendelea kuhamasisha jamii kijitokeza kupima VVU na kuhimiza kuanza kuchukua dawa za kufubaza makari ya virusi vya UKIMWI na kujikubali
Kuendelea kutoa elimu kwa jamii hasa kubadili tabia ili kuepukana na ugonjwa huu.
Mwisho:
Tunaamini kuwa Tanzania bila UKIMWI inawezekana endapo tukishiriana pamoja kama kauli mbiu inavyosema ya kwamba”Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI.
SUMBAWANGA
Anwani ya Posta: P.O.BOX 229
Simu ya Mezani: 025-2802133
Simu ya Kinganjani: 0754634811
Barua pepe: ded@sumbawangadc.go.tz
Hati Miliki©2017. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Haki zote zimehifadhiwa