Mh. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ndugu Kalolo Ntilla, jana 29 Julai 2019 amehitimisha maadhimisho ya sherehe ya Nanenane kwa mwaka 2019 ngazi ya Wilaya katika viwanja vya shule ya msingi Ilemba iliyoko kata ya Ilemba Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, kutumia fursa ya kutembelea katika maonesho hayo ili kujifunza mbinu mbalimbali za kitaalamu katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye maonesho hayo Mh. Mwenyekiti ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, aliwasihi wananchi wote kutumia fursa ya maonesho hayo kwa kuwatumia ipasavyo wataalamu ambao wapo katika viwanja hivyo ili kupata ushauri na maelekezo ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi kupitia Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Ushirika.
Alisema kuwa wananchi wanapaswa kutembelea katika maonesho hayo kwa lengo la kujifunza ili kuwa tayari kuanza kutumia teknolojia na maarifa watakayopata kwa lengo la kujiletea mapinduzi halisi katika kilimo, mifugo na uvuvi. Mhe Mwenyekiti alisema kuwa sekta ya kilimo nchini itaendelea kuwa sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususani katika wakati huu ambapo serikali imejidhatiti kufikia uchumi wa viwanda. Alisema sekta ya kilimo imeendelea kuimarika kwa kuchangia Pato la Taifa .
Sambamba na hayo pia aliwataka wataalamu wa kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha wanafikisha elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya kanuni za kilimo na ufugaji bora kulingana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Vile vile aliyataka makampuni ya pembejeo kuhakikisha yanaleta mbegu na mbolea bora tena kwa wakati muafaka wa msimu wa kilimo.
Kwa upande wa taasisi za Kelelimu zinazotoa elimu juu ya kilimo na mifugo ambazo zilikuwepo kwenye maonyesho ya nanenane ikiwemo chuo Kikuu cha MUST Tawi la Rukwa na kituo cha kilimo Laela, aliviomba kujitangaza zaidi ili wanafunzi wanaotoka kwenye Halmashauri ya Sumbawanga waweze kujiunga na vyuo hivyo kwa kuwa aliridhishwa na ubora wa kazi zao na elimu walioitoa kwa wakulima na wafugaji.
Mwisho, aliwataka wananchi kuzingatia elimu walioipata kwenye maadhimisho hayo ili kuweza kuepukana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwenye suala zima la kilimo na ufugaji. “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.
SUMBAWANGA
Anwani ya Posta: P.O.BOX 229
Simu ya Mezani: 025-2802133
Simu ya Kinganjani: 0754634811
Barua pepe: ded@sumbawangadc.go.tz
Hati Miliki©2017. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Haki zote zimehifadhiwa