Serikali imeziagiza Sekretarieti za Mikoa kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kukamilisha majibu ya hoja zote za ukaguzi za mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017, na kuwasilisha majibu hayo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya uhakiki kabla ya tarehe 30 Juni, 2018.
Maagizo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serekali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Ndugu Tixon Nzunda, wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi kutoka Seksheni za Mipango na Uratibu, pamoja na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Seksheni za Usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Sekretarieti za Mikoa, kilichofanyika Mei 4, 2018 katika Ukumbi wa Video Conference, OR-TAMISEMI.
Ndugu Nzunda ameyasisitiza hayo kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, kuwa Mikoa yote ni lazima sasa ijipange kuhakikisha inasimamia ipasavyo kazi ya kujibu hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili ifikapo muda uliotolewa na Serikali hoja zote za ukaguzi ziwe zimejibiwa ipasavyo na kuwasilishwa katika mamlaka husika.
Mbali na kuwaagiza kusimamia ipasavyo suala la kujibu hoja, Naibu Katibu Mkuu aliwaambia Makatibu Tawala hao wasaidizi juu ya mwenendo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19 ambapo alisema kuwa bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa iliandaliwa kupitia mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa (PlanRep Web Based), ambao umewezesha Halmashauri zote 185 kuwa namipango iliyoboreshwa.
Ndugu Zunda amewataka watendaji pia kusimamia kazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo iliyopo bila ya kuwaonea haya Wakurugenzi wa Halmashauri.
“Mkurugenzi kwa mujibu wa utendaji anawajibika kwa RAS, na wewe unapotekeleza majukumu yako unakuwa umevaa kofia ya RAS, hivyo sitegemei Katibu Tawala Msaidizi katika ngazi ya Mkoa atoe visingizio kuna Mkurugenzi anamkwamisha katika kutekeleza wajibu wake,” alisema Ndugu Nzunda, na kuongeza kuwa katika awamu ya sasa hakuna wa kuachwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake.
Naibu Katibu Mkuu amefafanua kwamba, kikao hicho watajadili kwa kina vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ambavyo ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya, Elimu na Maji, kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri, kuanzishwa kwa fursa za miradi ya kimkakati, maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, majengo ya utawala kwa Halmashauri mpya, sambamba na ununuzi wa magari ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya.
Maeneo mengine ya Bajeti ni ununuzi wa boti za kutolea huduma kwenye maeneo yenye changamoto za usafiri wa majini, kutenga maeneo ya uwekezaji, hususan viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya vijana na akina mama na watu wenye ulemavu, huku nguvu kubwa ikiwekwa katika sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi naukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa, OR TAMISEMI, Bibi Beatrice Kimoleta alisema kuwa Seksheni ya Mipango na Uratibu pamoja na Seksheni inayosimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa ni viungo muhimu katika suala zima la masuala ya mipango na bajeti.
“Lazima mtambue kwamba hizi idara mbili ninyi ndio injini ya Katibu Tawala Mkoa katika kumshauri juu ya masuala mazima ya mipango na bajeti. Kamwe huwezi kuzitenganisha idara hizi halafu ukafanikiwa, hivyo shabaha ya kuwaleta pamoja katika kikao hiki ni kutaka muwe na uelewa wa pamoja ili mtakapotoka hapa mkalete matokeo chanya kwenye Mikoa na Halmshauri zenu,” alisema Kimoleta.
“Katika mwaka wa fedha 2018/19, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepanga kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi 6,186,418,709,500. Kati ya fedha hizo, shilingi 298,346,001,000 ni kwa ajili ya Sekretarieti za Mikoa sawa na asilimia 5% na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetengewa shilingi 5,888,072,708,500 sawa na asilimia 95%” alisema Nzunda.
(Picha na habari na Atley Kuni)
SUMBAWANGA
Anwani ya Posta: P.O.BOX 229
Simu ya Mezani: 025-2802133
Simu ya Kinganjani: 255755023952
Barua pepe: ded@sumbawangadc.go.tz
Hati Miliki©2017. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Haki zote zimehifadhiwa